22/04/2026
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Ufugaji Yatembelea Viwanda vya Saruji, Mkoa wa Tanga – Aprili 2026
Shirikisho la Viwanda Tanzania (Confederation of Tanzania Industries (CTI) liliandaa ziara ya siku moja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Ufugaji, iliyoongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Deodatus Mwanyika, kutembelea viwanda vya Neelkanth Chemicals Limited, Yogi Polypack Limited na Tanga Cement Plc ambao ni wanachama wa CTI.
Lengo la ziara hiyo lilikuwa kuwapatia wajumbe wa Kamati fursa ya kujionea kwa vitendo maendeleo ya viwanda pamoja na changamoto zinazovikabili, ili kuimarisha utekelezaji wa sera na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Kupitia ziara hii, Kamati ilipata uelewa mpana kuhusu mchango wa sekta ya viwanda katika kukuza uchumi wa Taifa, ikiwemo uundaji wa ajira rasmi, uongezaji thamani wa malighafi za ndani, na nafasi ya sera thabiti katika kuvutia na kulinda uwekezaji endelevu.
Aidha, wamiliki na waendeshaji wa viwanda walipata jukwaa la kuwasilisha changamoto zao, ikiwemo masuala ya kikodi, ushindani wa bidhaa za ndani na nje, pamoja na masuala ya kiutendaji, na kutoa mapendekezo ya kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji. Wakati huohuo, walitambua jitihada za Serikali zinazoendelea katika kuboresha mazingira ya biashara.
Ziara hii pia ilisisitiza umuhimu wa kuwa na sera thabiti na zinazolingana, hususan katika maeneo ya kodi, pamoja na muingiliano wa sera kati ya sekta ya madini na viwanda vya saruji.
CTI inaendelea kuthibitisha nafasi yake k**a kiungo muhimu kati ya Serikali na sekta ya viwanda, kwa kuhimiza maamuzi ya sera yanayotegemea ushahidi na mahitaji halisi ya wazalishaji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga uchumi shindani, jumuishi, na unaoongozwa na uzalishaji wa ndani.