06/06/2026
DIT MWANZA YATOA ELIMU YA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA, WANAFUNZI WATAKIWA KUTOA TAARIFA MAPEMA
Wanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Mwanza leo, tarehe 6 Juni 2026, wamepatiwa elimu kuhusu kinga na namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kupitia semina iliyofanyika katika viwanja vya kampasi hiyo, ikihusisha wataalamu kutoka Hospitali ya Sekou Toure, Dawati la Jinsia pamoja na Jeshi la Polisi Kirumba.
Akifungua semina hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa DIT Kampasi ya Mwanza na Mratibu wa Dawati la Jinsia wa Mradi wa EASTRIP, Bi. Doris Ngogo, amesema kuwa utoaji wa elimu hiyo ni muhimu kutokana na mwingiliano wa watu wenye malezi na mitazamo tofauti chuoni.
"Tutaendelea kutoa elimu hii ili kujenga mazingira salama ya kujifunzia na kufanya kazi, huku tukiwahamasisha wanafunzi kutoa taarifa mapema wanapokumbana na vitendo vya ukatili," amesema Bi. Ngogo.
Akizungumza kwa niaba ya Kituo cha Pamoja cha (One Stop Center) Afisa Ustawi wa jamii kutoka Hospitali ya Sekou Toure, Bwana Salum Mwanaki ameleza kuwa wahanga wa ukatili wanaweza kupata huduma zote muhimu katika eneo moja ikiwemo matibabu, msaada wa kisaikolojia, ustawi wa jamii, usaidizi wa kisheria na huduma za Polisi Rafiki.
Dkt. Charles Makoye amewasisitiza wanafunzi kutafuta huduma za kitabibu haraka baada ya kufanyiwa ukatili.
"Mtu anayefanyiwa ukatili wa kingono anapaswa kufika hospitali ndani ya saa 72 ili kupata tiba na kinga dhidi ya maambukizi mbalimbali ikiwemo VVU," amesisitiza.
Naye Leah Ogutu Polisi rafiki kutoka Kituo cha Polisi Kirumba amewahimiza wanafunzi kutovumilia vitendo vya ukatili na kutoa taarifa bila hofu.
Wakizungumza kwa niaba ya wanafunzi, Notorian Nicholaus na Vivian Reuben wameishukuru Menejimenti ya DIT kwa kuandaa semina hiyo, wakieleza kuwa imewaongezea uelewa kuhusu haki zao na namna ya kujikinga dhidi ya vitendo vya ukatili.
"Tumejifunza umuhimu wa kutoa taarifa mapema na kutafuta msaada bila kuogopa. Elimu hii itatusaidia kufanya maamuzi sahihi katika maisha yetu ya chuoni," wamesema.